Spika: Waliofungua Kesi ya Bandari, wameangukiwa na kitu kizito

Baada ya uamuzi wa mahakama kuhusu kesi ya mzozo wa bandari kutolewa kwa kampuni ya DP World yenye makao yake Dubai, mahakama iligundua hakukuwa na kosa lolote kuhusu mikataba. Kesi hiyo iliyosikilizwa Mbeya.

Spika wa Bunge la Tanzania, akiwa katika ziara ya kutembelea jimbo lake la Mbeya Mjini siku ya jana, aliwahakikishia wananchi kuwa bandari haijauzwa na waliofungua kesi hiyo walishindwa mahakamani. Alieleza:

“Leo (jana) hukumu ya kupinga mkataba wa bandari imetoka lakini kabla haijatoka, nilishafanya mikutano kadhaa nikawaambia wana-Mbeya mjini kuwa bandari haijauzwa. Nilisema, ‘Je, nchi imeuzwa? Mtu akikuambia bandari imeuzwa, mwambie shilingi ngapi?’ Akishindwa kujibu, basi jua ameshindwa kabisa! Kwa sababu leo (jana) watu wamepata ufahamu, sasa wameelewa. Na wewe mwana-Mbeya mjini, elewa mimi ni Mbunge wako.”

Hapo awali, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ilifuta kesi inayopinga mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai. Mahakama ilithibitisha kuwa mkataba huo wa IGA ulikuwa halali na haikuwa na msingi wa malalamiko yaliyowasilishwa.

Uamuzi huo ulitolewa katika kesi namba 5 ya mwaka 2023 iliyofunguliwa na mawakili Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde, na Frank Nyalus. Jopo la majaji watatu, chini ya Jaji Dastan Ndunguru, lilitathmini hoja na kufikia uamuzi kuwa hoja zilizotolewa hazikuwa na msingi, hivyo mkataba wa IGA ulikuwa halali na haukuwa na kasoro zinazosababisha usitishwe.

Kwa mujibu wa malalamiko, mkataba huo ulikuwa na misingi minne ya kisheria: kutoridhiwa kwa umma na kutokuwashirikisha wananchi kabla ya kuridhiwa, tuhuma za mkataba kukiuka sheria, mkataba kuonekana kuwa kinyume na maslahi ya umma na rasilimali za umma, pamoja na kuwa na vifungu vinavyoonekana kuwa na uwezo wa kuhatarisha usalama wa nchi. Kwa kujibu kauli hiyo, Wakili wa walalamikaji, Bonifasi Mwabukusi, alieleza nia ya kukata rufaa, kwa kuwa hawakukubaliana na uamuzi wa mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *