Kesi ya kwama, mahakama yashindwa kulipa mashahidi

Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake, kwa sababu mahakama imeshindwa kuwalipa stahiki zao mashahidi watano wa upande wa mashtaka.

Madai hayo yalitolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo illipoitwa leo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Wakili Mbagwa amedai kuwa kesi hiyo leo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini wameshindwa kuwaita mashahidi wengine kwa sababu shahidi wa 9,10,11,12 na 13 ambao tayari walishatoa ushahidi wao bado hawajalipwa stahiki zao na kuiomba mahakama itoe amri kwa uongozi wa Mahakama ili mashahidi hao waweze kulipwa stahiki zao.

Hakimu Simba alisema watalitatua tatizo hilo sababu kesi hiyo ni ya muda mrefu na kwamba walikubaliana waletwe mashahidi wa kutosha ili kesi imalizike haraka.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 17 mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na itaendelea kusikilizwa Juni 18, 20 na 24.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Gugai na mwenzake watatu wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo, makosa 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *