Samia agoma kuongeza muda katika matumizi ya mifuko ya plastiki

Image result for samia suluhu photos

Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu amesema serikali haitaongeza muda wa matumizi ya mifuko ya plastiki huku akipiga marufuku matumizi ya maji maarufu ya ‘Kandoro’ yanayohifadhiwa katika mifuko midogo laini kwa sababu haijathibitishwa usalama wake na pia inachafua mazingira.

Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kikao cha viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.

Alisema zipo picha ambazo zinasambazwa katika mitandao ya kijamii, watu wakilinganisha mifuko ya plastiki na ya karatasi lengo likiwa ni kuishawishi serikali kuongeza muda wa matumizi ya mifuko hiyo.

Image result for samia suluhu photos

“Watu wanaoanisha picha za mifuko ya plastiki na ya karatasi, kuna mtu mkono mmoja ameshika mifuko ya plastiki ikiwa mingi na mkono mwingine ameshika mifuko ya karatasi ikiwa michache, picha nyingine zinaonyesha shefu za mifuko mbadala zikiwa tupu na mingine ni mingi, haya yote ni kuishawishi serikali iongeze muda wa matumizi ya mifuko hiyo,”alisema Samia Suluhu na kuongeza:

“Nataka kuwaambia ndugu zangu hatutaongeza muda, ifikapo Juni mosi hakuna mfuko wa plasitiki kuonekana na katika hili hakuna kubembelezana, tumeshasema sana tangu mwaka 1991, naomba sasa tutekeleze na Dar es Salaam ndiyo kigezo, tukifanya vizuri hapa mikoa yote itafanya vizuri kwa sababu huu mkoa ndiyo msambazaji mkubwa wa mifuko hii ya plastiki, na Dar es Salaam ndiyo Tanzania yenyewe.”

Pia Makamu wa Rais aliliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuharakisha utoaji wa vibali kwa viwanda vya uzalishaji wa mifuko hiyo mbadala ili waanze uwekezaji haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *