Wanafunzi Waponea Chupu Chupu baada ya Paa la Darasa Kubebwa na Upepo Mkali

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Gitwebe katika eneo bunge la Mugirango Kaskazini, Kaunti ya Nyamira Jumanne walinusurika kifo baada ya paa, milango na madirisha ya  madarasa kung’olewa na kubebwa na upepo mkali.

Makamu wa mwalimu mkuu katika Shule hiyo, Eunice Nyarango, alilalamikia kudorora kwa majengo ya madarasa hayo akisema kwamba wanafunzi hao 150 walikuwa na bahati kuwa tukio hilo lilitokea baada ya masomo kumalizika jioni.

Nyarango alielezea kuwa upepo mkali umekuwa tishio kwa usalama wa watoto kwa muda sasa.

“Wakati kunaelekea kunyesha, tunalazimika kuwaachilia wanafunzi kwenda makwao kama tulivyofanya kabla ya tukio hili ili kuzuia majanga,” alisema Nyarango.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Gitwebe Simon Nyangacha alisema kuwa shughuli za kujifunza sasa zinafanyika chini ya miti.

Mkuu wa shule hiyo Zefan Omboto alisema kwamba hofu imeenea kwa shule nzima kwani vyumba vingine vya madarasa pia vina hatari ya kuporomoka kutokana na upepo mkali.

Vyumba vya madarasa matatu na ofisi moja ziliathiriwa na tukio hilo ambalo limekutokea siku moja baada ya wanafunzi wanane kupoteza maisha yao na wengine wengi kupone na kuuguza majeraha katika Shule ya Precious Talents jijini Nairobi kufuatia kuporomoka kwa ukuta wa vyumba vyao vya darasa.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa elimu George Magoha aliahidi kujenga shule mpya kwa wakaazi wa Ngando baada ya janga lililotokea katika Chuo cha Precious Talents.

Magoha hapo awali alitupila mbali madai kuwa hakukuwa na Shule ya umma katika eneo hilo. Alifafanua kuwa shule ya umma ilikuwa katika umbali wa kilomita mbili, hata hivyo katika kata tofauti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *