Tutahesabiwa Mbinguni!- Mchungaji awazuia Maafisa wa Sensa Kuwahesabu

Image result for census kenya

Mchungaji wa WaKorino na mkewe wamekamatwa huko Naivasha baada ya kuwazuia waandikishaji wa sensa kuwahesabu.

Kisanga hicho kilitokea katika kijiji cha Gatamaiyu kilometa 30 kutoka mji wa Naivasha. Wawili hao na watoto wao wanne walitoa kizaazaa kabla ya polisi kuingilia kati.

Familia hiyo wakati mmoja ilijifungia chumbani na kupuuza masharti ya polisi ya kufungua mlango hadi pale  wazee wa eneo lile walipoingilia kati.

Wakinukuu sehemu za Bibilia, watuhumiwa waliotambuliwa kama Akhi Shilton na Akol Emmah walisema kwamba watahesabiwa mbinguni na sio duniani.

Mchungaji huyo aliwatishia waandikishaji wa sensa na maafisa wa polisi kuwa watalaaniwa kwa kufanya kinyume na Bibilia “ambayo inalaani aina yoyote ya sensa.”

“Kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati 2:17 kinatuzuia kuhesabiwa na hivyo hatutakubali kuchafua jina la Mungu ili kuifurahisha serikali au binadamu yeyote,” alilalamika Akhi.

Mzee wa eneo hilo anayetambuliwa kama Musa alisema kwamba si mara ya kwanza familia hiyo kuhusika kwenye mzozo wa kidini. Musa alisema kwamba hapo mbeleni walikuwa wamekataa watoto wao wapewe chanjo dhidi ya magonjwa.

“Katika visa vingi imewalazimu polisi kuingilia kati ili watoto wao wapewe chanjo. Hatujashangaa alipowazuia maafisa wa sensa, “alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *