Serengeti Kinara Afrika

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda tuzo ya kuwa hifadhi bora katika bara la Afrika kwa mwaka 2019, tuzo hiyo imetolewa nchini Mauritius na Taasisi ya World Travel Awards ambao ni waandaaji wa tuzo hizo kila mwaka.

Taarifa iliyoandaliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa mawasiliano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Pascal Shelutete imesema, washindi katika tuzo hizo hupigiwa kura na wabobezi katika masuala ya safari na utalii duniani kote.

Ushindi wa Serengeti, unatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na TANAPA katika kuzisimamia vyema hifadhi kwa kuzitangaza ili kuvutia wataliiwengi zaidi nchini.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayopita katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mara na Shinyanga ni eneo pekee duniani lenye kundi kubwa la wanyama wanaohama katika mfumo mzima wa mlishano, hifadhi hiyo pia inapakana na nchi ya Kenya.

Umaarufu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti unatokana na kuwa na misururu mirefu ya nyumbu wanaohama kwa makundi na kuvuka hata mpaka wa Tanzania hadi hifadhi ya wanyama pori ya Maasai Mara nchini Kenya.

Takwimu za TANAPA zinaonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya nyumbu milioni moja, pundamilia 200,000, swala tomi zaidi ya 300,000 na pofu 12,000 huunga misafara ya kutafuta malisho na maji

Inasemekena kuwa, neno Serengeti linatokana na neno la kimasai la sirenget lenye maana ya uwanda mpana wa nyasi fupi, malisho mengi na maji ya kutosha. Hifadhi hiyo, inapewa majina mengi kama vile lulu, bustani ya Afrika na Edeni ya Afrika kutokana na utajiri wa maliasili uliopo ndani ya hifadhi hii.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 ilianzishwa mwaka 1951, ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa nchini ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *