Kindoki mbioni kuondoka Yanga, klabu hii ya Tanzania inamuwinda

Klaus Kindoki

Taarifa kutoka ndani ya Walima Alizeti, Singida United zinaeleza kuwa klabu hiyo ipo mbioni kuwania huduma ya mlinda lango wa Yanga Mkongomani Klaus Kindoki kwaajili ya kuimarisha eneo la golikipa kutokana na kukosekana kwa kipa mahiri kwa sasa klabuni hapo.

Licha ya Kindoki kupewa nafasi kubwa ya kuanza katika klabu ya Yanga msimu huu uliomalizika, mlinda lango huyo hajawa na msimu mzuri sana hasa kutokana na wakati mwingine kuruhusu kufungwa mabao rahisi hali iliyosababisha Yanga kutafuta mbadala kwaajili ya kujiimarisha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Singida United, Cales Katemana, bado kwa sasa mipango yao hawajaweka wazi hasa kwa upande wa usajili kutokana na kusubiri ripoti ya mwalimu.

“Suala la usajili kwa timu yetu kwa sasa michakato haijaanza, ripoti ya mwalimu ikipita tutafanyia kazi mapendekezo yake hivyo kwa sasa mambo bado,” amesema amenukuliwa na Saleh Jembe.

Faruk Shikalo

Endapo dili la Kindoki litakamilika basi mlinda mlango huyo atabaki kwenye ligi msimu huu akiwa na kikosi cha Singida United ambacho kilikuwa kwenye hatihati ya kushuka daraja msimu uliopita.

Yanga wako mbioni kumwachia Kindoki huku ikielezwa kuwa tayari wamemalizana na mlinda lango kutoka Bandari ya Kenya Faruk Shikalo pamoja na kipa wa mbao Metacha Mnata ambao ndiyo wanatarajiwa kuchuana katika nafasi hiyo.

Kwa takribani msimu mzima uliopita Yanga walikuwa hawana matumaini inapofikia eneo la golikipa kutokana na kukosa kipa mahiri, ikizingatiwa kwamba Ramadhan Kabwili uzoefu wake bado mdogo huku Kindoki akiwa na makosa mengi ya kiufundi.

Ramadhan Kabwili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *