Lusekelo: Hakuna haja ya chaguzi wa serikali za mtaa

Askofu wa Kanisa la Maombezi la Gospel Riverval Center (GRC), Antony Lusekelo, maarufa kama Mzee wa upako, amesema serikali haina haja ya kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu kwani ni matumizi mabaya ya muda na fedha.
Askofu Lusekelo, aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu maendeleo ya nchini na juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli.
“Tungeacha nchi itulie, tufanye kazi, ningekuwa mimi, kama ambavyo Bwana mkubwa (Rais Magufuli) amekuwa akifuta sherehe mbalimbali za serikali, uchaguzi huu ningeufuta na ninaomba waufute, hauna tija kwa nchi yetu,” alisema Askofu Lusekelo.
Alipendekeza kuwa chaguzi zingefanyika kwa wakati mmoja badala ya kuanza kufanya chaguzi kwa miaka miwili mfululizo, kuna sababisha shughuli za maendeleo kukwama.
Alisema angepata fursa ya kumshauri Rais Magufuli, angemshauri kufuta uchaguzi huo na viongozi waliopo waendelee na shughuli zao hadi hapo utakapotangazwa uchaguzi mkuu ujao.
“Uchaguzi ufanyike mara moja, ikifika mwakani uanze uchaguzi wa Serikali za Mitaa, madiwani, wabunge na Rais ili tuache shughuli za maendeleo zifanyike,” alisema Askofu Lusekelo.
Alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, kumshauri Rais Magufuli ili afute uchaguzi huo na badala yake ufanyike mwakani na viongozi waliopo madarakani waendelee kutekeleza majukumu yao.
Sabamba na hilo, aliwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika utekelezaji wa majukumu yake hasa kukuza uchumi wa Taifa.
Alisema amefanya kazi nyingi hivyo anapaswa kupewa muda wa kuendelea kuzifanikisha katika kipindi chake za uongozi.
“Sisemi haya kwa sababu najipendekeza sina shida na ukuu wa wilaya wala kitu kingine, ninayoyasema mtakuja kuyakumbuka miaka ijayo,” alisema Askofu Lusekelo.
Alisema kwa tathimini yake, miongoni mwa nchi zitakazokuwa na maisha mazuri miaka mingi ijayo, Tanzania ni miongoni.
Aidha, Askofu Lusekelo alisema haungi mkono wanasiasa wanaohama vyama kwa sababu yoyote ile kwa sababu ni kuwapotezea muda Watanzania.
Alisema watu wa aina hiyo, hawana misimamo na wanadhihirisha uongo wao kwa madai ya kuhama vyama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *