Bei za taulo za kike bado hazijabadilika sokoni

 

 

Wizara ya Fedha na Mipango imesema licha ya serikali kuchukua hatua ya kuondoa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike, imebainisha kuwa hakuna mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo sokoni.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Ashatu Kijaji alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum(Chadema), Sophia Mwakagenda.

Katika swali lake, Mbunge huyo alisema katika bajeti ya mwaka 2017/18 serikali iliondoa kodi hiyo lakini mpaka sasa ni mwaka mmoja bei ya taulo za kike haijashuka.

“Je, ni lini serikali itasimamia kwa ukamilifu suala hili ili bei za taulo za kike zishuke na kusaidia afya za wanawake, hususan wasichana,”alihoji.

 

Akijibu swali hilo, Dk.Kijaji alisema gharama hizo ni pamoja na malighafi, mishahara, uwekezaji, mifumo ya uzalishaji, teknolojia, ushindani katika soko, umeme, maji na maji taka, usambazaji, ubora wa bidhaa.

“Kutokushuka kwa bei ya taulo za kike kunabainisha kwamba, kodi inachangia kwa sehemu ndogo sana katika kupanga bei ya bidhaa, kama ambavyo serikali imekuwa ikisisitiza na kutoa ufafanuzi mbele ya Bunge,”alisema.

Aidha, alisema kwa sasa mfumo wa uchumi ni mfumo wa soko huria na bei ya bidhaa huamuliwa na nguvu ya soko, yaani ugavi na mahitaji ya soko.

“Fursa pekee iliyopo ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa wa kutumia teknolojia yenye gharama nafuu katika kutengeneza taulo za kike, kupunguza gharama nyingine, sambamba na kuchochea ushindani wa bei katika soko na siyo kuondoa kodi na kupanga bei ya bidhaa,”alisema.

Katika swali lake la nyongeza, Mbunge huyo alihoji mkakati wa serikali ina mpango gani wa kuweka bei elekezi kwenye taulo hizo.

Akijibu swali hilo, Dk.Kijaji alisema hakuna ulazima wowote wa kuweka bei kwenye bidhaa hizo kwasababu wapo kwenye soko huria serikali haitaki kuingilia jambo hilo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *