Usajili wa Ndemla, Yanga umefikia hapa

KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya Simba, Said Hamisi Ndemla, amesema kwa sasa akili yake ameelekeza kucheza soka nje ya nchi na hivyo suala la yeye kwenda Yanga halina haraka isipokuwa akiona kuna ulazimabasi atasaini.

Ndemla ambaye anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kupiga mashuti licha ya mwili wake kuwa mdogo amekuwa akipata nafasi mara chache sana katika timu yake ya Simba, hali inayomsukuma kutaka kuondoka klabuni hapo.

Ikumbukwe kuwa msimu huu, Ndemla alipewa ruhusa na Simba ya kwenda kufanya majaribio katika timu ya Eskilstuna ya Sweden, ambapo mpaka sasa hayajawahi kutolewa majibu yenye uhakika juu ya matokeo ya majaribio hayo.


Ndemla alisema pamoja na mkataba wake kufikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu, hana haraka ya kuongeza mpya, hadi hapo dili lake la kwenda kucheza nje ya nchi litakaposhindikana.

“Sina mpango wa kusaini Simba mapema hii, zaidi najipanga kuangalia dili langu la kucheza nje ya nchi, endapo nitakwama basi nitakuwa tayari kusaini Yanga au kuongeza mkataba Simba kama watakuwa bado wanahitaji huduma yangu,” Ndembe ameuambia mtandao wa Saleh Jembe.

“Tetesi zote ambazo zimekuwa zikisemwa juu yangu naweza kusema zitabaki kuwa tetesi ila mipango kamili naijua mwenyewe, japo nasikia kuna watu wanazusha eti kuwa nilitolewa kambini kisa niligoma kusaini Simba, hilo si kweli, mimi ninaumwa sasa ni wiki nipo tu nyumbani naendelea na matibabu,” alisema Ndemla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *