Anayedaiwa kumteka MO afikishwa mahakamani leo


DEREVA Taksi ambaye ni Mkazi wa Tegeta , Mousa Twaleb (46), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kumteka nyara Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu kwa jina la MO.

Twaleb amefikishwa mahakamani hapo leo asubuhi na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai katika shitaka la kwanza mshitakiwa alijihusisha na genge la uhalifu.

Kadushi alidai Mei 1 na Oktoba 10, mwaka 2018 katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.

Alidai Oktoba 11, mwaka jana eneo la Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

 

Wakili Simon alidai Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Hakimu Shaidi alisema mshitakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Wakili Kadushi alidai sehemu kubwa ya upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo wanafuatilia taratibu za kisheria ili shauri hilo liweze kusikilizwa.

Mshitakiwa Twaleb alidai anaomba dhamana kwa sababu alikuwa nje.

Hakimu Shaidi alisema makosa hayo ya uhujumu uchumi hayana dhamana kisheria na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 11, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa alirudishwa rumande.

MO alitekwa Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo majira ya usiku alipotelekezwa na gari katika eneo la Gymkhana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *