Mustakabali wa Kwasi ndani ya Simba ‘wasiwasi’

Beki wa kushoto wa Simba Mghana Asante Kwasi, ameonesha dhamira ya kuendelea kubaki kwenye klabu yake ya Simba na kupambania namba yake kuliko kutolewa kwa mkopo.

Kwasi ambaye anasifika kwa matumizi yake ya nguvu akiwa uwanjani kwa sasa amekosa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza hali inayompa wasiwasi wa kuendelea kubakia klabuni hapo.

Kwasi alijiunga na Simba kwenye dirisha dogo la usajili msimu uliopita akitokea Lipuli FC ya Iringa, kwa mkataba wa miaka miwili ambapo mkataba wake unatarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu, huku mchango wake ndani ya klabu hiyo ukiendelea kuwa mdogo zaidi.

Kwasi alisema, pamoja na mkataba wake wa kuitumikia Simba kubakiza miezi mitano tu, hatakubali kuiacha kizembe hata kama viongozi wake watataka kumtoa kwa mkopo.

“Napenda sana kuendelea kuitumikia Simba kwa msimu ujao, pamoja na kuwa na muda mfupi wa kucheza kwa sasa.

“Siko tayari kuiacha Simba, ila nitajitahidi kupambana kadiri ninapopewa nafasi za kucheza na kocha ili nionyeshe mchango hasa kwa msimu ujao kwani msimu huu umekuwa mgumu kwangu baada ya kukabiliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Kwasi yupo pamoja na Waghana wenzake katika klabu ya Simba ambao ni Nicholous Gyan pamoja James Kotei. Kati ya hao watatu, Kotei pekee ndiyo ameonekana kuwa na namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *