Hii ndiyo orodha ya wachezaji 14 wa Yanga ambao mikataba yao imekwisha

Changamoto kubwa inayowakabili viongozi wa Yanga kwa sasa ni kuhakikisha wachezaji wao wote waliomaliza mikataba wanapewa mikataba mipya na kuongeza wachezaji wengine wapya ambao wataleta changamoto mpya katika timu hiyo kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.

Changamoto hiyo imekuja kufuatia idadi kubwa ya wachezaji wa timu hiyo kumaliza mikataba yao na hivyo kuwa wachezaji huru huku kukiwa na taarifa baadhi yao kuwa mbioni kujiunga na timu nyingine.

Hali hiyo imekuja kutokana na klabu hiyo kuyumba kwa kiasi kikubwa katika masuala ya kifedha, iliyochagizwa na kukosekana kwa uongozi imara na thabiti kwa muda mrefu hususan tangu alipojiuzulu aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo Yusuf Manji.

Sasa uongozi mpya wa klabu hiyo upo kwenye mchakato wa kuboresha mikataba ya wachezaji wao kwa kuhakikisha wanakuwa na muda mrefu kwa hofu ya kujitokeza kama ya kiungo wao mshambuliaji, Ibrahim Ajibu..

Ajibu ni kati ya wachezaji 14 wanaotarajiwa kumaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu (Mei 28), na kiungo huyu fundi anatarajiwa kwenda TP Mazembe ya DR Congo ambayo imeshamtangazia ofa nono.

Lakini kiungo huyo atajiunga na Mazembe kama mchezaji huru, baada ya Yanga kujisahau hadi kushtukia anamaliza mkataba wake, kwa hiyo haitaambulia hata shilingi kutoka kwa nyota huyo kama akimalizana na Wacongo hao.

Suala hilo limeishtua Yanga na kuamua kuboresha mikataba ya wachezaji wao muhimu akiwemo kiungo mkabaji tegemeo, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu ni Ramadhani Kabwili, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Pato Ngonyani, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu, Said Juma na Matheo Anthony.

Wengine ni Mrisho Ngasa, Thabani Kamusoko, Papy Tshishimbi (ameongeza), Raphael Daudi, Pius Buswita, Juma Mahadhi, Baruani Akilimali, Amissi Tambwe, Haruna Moshi na Ajibu mwenyewe.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *